UTANGULIZI
Idara ya utamaduni ni moja kati ya Taasisi zilizomo katika Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Idara hii imeundwa ili ihakikishe kwamba Urithi wa Utamaduni wa Zanzibar unaendelezwa na kudumishwa kwa maendeleo na ustawi wa Taifa la Zanzibar na wananchi wake sambamba na Kuwa na utamaduni na sanaa inayowaendeleza wasanii ili kuweza kujiinua kiuchumi na kupunguza umasikini kwa kutekeleza majukumu yake ya msingi ambayo ni Kufufua, kulinda, kuimarisha pamoja na kuendeleza utamaduni wa Zanzibar kwa faida na maslahi ya jamii ya Wazanzibar, kiuchumi na kisiasa ili kwenda sambamba na soko la kazi za sanaa na uhifadhi wa utamaduni bila ya kuathiri silka na desturi za Mzanzibari. pamoja na kuifanya michezo kuwa ni sehemu ya ajira na kujenga afya.
Idara ya Utamaduni hufanya kazi kwa kushirikiana na Mabaraza yalio chini yake ambayo kimsingi yamepewa jukumu la kutekeleza Sera ya Utamaduni kwa kutumia uwezo na nguvu za kisheria walizopewa chini ya mabaraza yao; Baraza la Sanaa, Sensa ya Filam na Utamaduni (BASSFU) na Baraza za Kiswahili Zanzibar (BAKIZA). Aidha Idara ya Utamaduni ina vitengo viwili inavyovisimia navyo ni:- a) Nyumba ya Sanaa iliopo Mwanakwerekwe na Studio ya Filam na Muziki iliopo Rahaleo.
DIRA
Zanzibar kuwa na utamaduni ulioimarika kwa kukuza na kuendeleza nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa ifikapo 2030.
DHAMIRA
Kuratibu shughuli za Utamaduni wa wananchi wa Zanzibar kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho katika kusimamia na kuinganisha jamii yenye maadili ili kuimarisha umoja na mshikamano na kuhamasisha maendeleo ya kiuchumi na kulitambulisha Taifa ndani na nje ya nchi.
MATANGAZO
"Mwaka wa 2024 tushirikiane kurejesha maadili yetu katika Familia zetu"
DHANA ZA UTAMADUNI
MILA

Dhana hii hujumuisha vipengele vya malezi, tiba za asili, mazindiko, ramli na utabiri, kinga, harusi, vifo, mirathi na kadhalika Huu ni muhimili mwengine wenye nguvu katika kuelezea utamaduni wa Zanzibar. Kupitia mila jamii inapata uwezo wa kuufufua, kuuhuisha, kuimarisha, kuuenzi na kuuendeleza utamaduni wao.
DESTURI

Kipengele hiki huhusisha kawaida za jamii kama vile; maamkizi, kutembeleana, kusaidiana, hishima, adabu na maadili mema. Kwa ujumla desturi inapojikita na kuimarika katika jamii hugeuka na kuwa mila. Ndipo Waswahili wakasema Kawaida ni kama sheria.
ITIKADI

Kipengele hiki huhusisha mambo ya imani za kiroho, kijadi na kisiasa. Masuala ya ibada, tambiko na mizimu zinaingia katika uwanja huu.
SANAA ZA ASILI

Hii hujumuisha shughuli zote zinazofanywa na binaadamu kwa kutumia ustadi wake. Kwa ujumla, sanaa hugawiwa katika mafungu makuu matatu: sanaa za maonesho, sanaa za ghibu kama muziki wa ala tupu na sanaa ya utendaji (uhandisi) ambazo tumezowea kuziita sanaa za ufundi.
MAVAZI YA MZANZIBARI

Kipengele hiki kinajumuisha mavazi ya aina mbali mbali wanayotumia katika shughuli za jamii ya Wazanzibar kutokana na maendeleo ya jamii na maingiliano ya watu wetu na mataifa mengine Mavazi kama baibui la uzi na kanga kwa wanawake na kanzu na kofia za kiua na koti kwa wanaume yamekuwa yakiutambulisha utamaduni wetu.
LUGHA

Kipengele hiki kinajumuisha lahaja zote za lugha ya kiswahili ambayo jamii inazitumia katika mawasiliano na fasihi zote mbili andishi na simulizi ambazo ni zao la jamii yenyewe inayohusika na mila za watu.